Alhamisi 5 Novemba 2026 - 08:25
Ufuatiliaji wa Kisheria wa Jinai za Marekani na Utawala wa Kizayuni Unapaswa Kutoka Kwenye Mikutano na Kuelekea Kwenye Hatua za Vitendo

Hawza/ Sheikh al-Nasiri huku akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za vitendo katika kufuatilia jinai zinazofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni, amesema kuwa; uwekaji wa kumbukumbu za jinai hizo, uandaaji wa mashauri ya kisheria na uwasilishaji wa malalamiko katika mahakama za ndani na za kimataifa vinapaswa kuchukua nafasi ya mikutano na makongamano yanayoishia katika mijadala ya kinadharia pekee.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Mashhad, Sheikh Yusuf al-Nasiri, miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Muqawama nchini Iraq, alisisitiza umuhimu wa kugeuza uwezo uliopo katika nyanja za sheria na mahusiano ya kimataifa kuwa hatua za vitendo zitakazowezesha kuwafikisha mahakamani wahusika wa jinai zinazofanywa dhidi ya mataifa yanayodhulumiwa.

Alitoa kauli hiyo katika jopo maalumu lililojadili mbinu za kuweka kumbukumbu na kufuatilia kisheria jinai za adui wa Marekani na Mzayuni. Jopo hilo lilifanyika pembezoni mwa mkutano wa Mujahidina Walio Uhamishoni, katika ukumbi wa Sheikh Baha'i wa Taasisi ya Utafiti wa Kiislamu ya Haram ya Imam Ridha (as).

Akikosoa tabia ya mikutano na makongamano mengi ya kisheria kuishia katika kuwasilisha mitazamo na kutoa matamko, alisema: Ili kufikia matokeo, shughuli za kisheria zinapaswa kuvuka hatua ya kauli mbiu na mazungumzo, na kuelekea katika utekelezaji wa hatua za vitendo pamoja na ufuatiliaji endelevu katika taasisi za kimahakama za kimataifa.

Sheikh al-Nasiri, ambaye ni mwanasheria na mshauri wa mashirika ya kimataifa, alirejelea uzoefu wake katika uwanja wa sheria za kimataifa, ukiwemo ushirikiano wake na taasisi kama vile Shirika la Msalaba Mwekundu, alisema kuwa; licha ya kufanyika mikutano na makongamano mengi nchini Iran kuhusu jinai za maadui, sehemu kubwa ya programu hizo haijaishia katika matokeo ya vitendo wala kufuatiwa na hatua za kimahakama.

Sheikh al-Nasiri amesema kuwa; tangu miaka ya mwanzo baada ya kuuawa kishahidi Kamanda Hajj Qasem Soleimani, amekuwa akiwahimiza viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatilia kisheria jinai hiyo katika mahakama za ndani na za kimataifa.

Aliongeza kuwa; ni lazima kuandaa mashauri ya kisheria kwa kushirikiana na familia za mashahidi pamoja na taasisi za mahakama, kisha kuyafuatilia kupitia njia za kisheria katika nchi mbalimbali.

Akizungumzia juhudi zake za kuzikusanya familia za mashahidi wa mhimili wa Muqawama na kuzihamasisha kuwasilisha malalamiko katika mahakama za maeneo wanayoishi, alisisitiza kuwa; ufuatiliaji wa kisheria haupaswi kuishia katika kuandaa mikutano na kupiga picha za kumbukumbu, badala yake kila shauri linapaswa kuwa na njia maalumu ya kimahakama na kiutekelezaji.

Mwanaharakati huyo wa Muqawama wa Iraq, akirejelea kukiri hadharani kwa Donald Trump kwamba alitoa amri ya kuuawa Kamanda Hajj Qasem Suleimani na wenzake, alisema kuwa kauli hiyo ni miongoni mwa vielelezo muhimu vinavyoweza kutumiwa katika kufuatilia jinai hiyo kisheria.

Alisisitiza kuwa kukiri wazi wahusika wa jinai kunaweza kutumiwa kama ushahidi katika mchakato wa kuandaa mashauri ya kisheria na kuthibitisha uwajibikaji wao wa kijinai.

Vilevile, akizungumzia jinai ya shambulio dhidi ya shule ya Shajarat Tayyibah, alirejelea kauli za afisa mmoja mwandamizi wa Jeshi la Wanamaji la Marekani kuhusu onyo lililotolewa kabla ya shambulio hilo dhidi ya shule hiyo.

Alieleza kuwa afisa huyo alikuwa amesema kuwa kabla ya kurushwa kombora, alitoa onyo kuhusu aina ya eneo lililolengwa na uwepo wa wanafunzi ndani yake, huku akionyesha wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa shambulio kutokea. Hata hivyo, licha ya onyo hilo shambulio la pili pia lilitekelezwa.

Sheikh al-Nasiri aliyataja matamshi hayo kuwa ni miongoni mwa ushahidi unaopaswa kuchunguzwa katika shauri la kisheria kuhusu jinai hiyo. Aidha, alikosoa kutokuwepo kwa ufuatiliaji wenye ufanisi na kusisitiza umuhimu wa kukusanya vielelezo na kuviwasilisha katika vyombo vya mahakama za kimataifa.

Akirejelea hatua iliyochukuliwa na Afrika Kusini ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki za binadamu, alisema kuwa; hatua hiyo ilifungua njia kwa nchi nyingine kujiunga na kuwaunga mkono kisheria na kisiasa kwenye malalamiko dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni. Alieleza kuwa hatua hiyo imeonesha kuwa ufuatiliaji wa kimahakama unaweza kuchangia kujengwa kwa mwafaka wa kimataifa dhidi ya wahalifu.

Mwanasheria huyo wa Iraq, akizungumzia mwitikio wa kimataifa dhidi ya jinai zinazofanyika Ghaza na kutengwa kisiasa na kimataifa utawala wa Kizayuni, alibainisha kuwa: Mabadiliko ya hivi karibuni yanaonesha kuwa maoni ya umma na misimamo ya nchi nyingi duniani kuhusu jinai za utawala huu yamebadilika, kwa hiyo tunapaswa kutumia fursa hii kuimarisha hatua za kisheria.

Mhimili wa Muqawama Unahitaji Mkakati Unaovuka Mipaka ya Kijiografia

Sheikh al-Nasiri, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mtazamo wa kimkakati katika kushughulikia masuala ya mhimili wa Muqawama, alisema: Hatupaswi kuchambua masuala ya eneo hili kwa kuzingatia tu mipaka ya kijiografia ya nchi mbalimbali, kwa sababu matukio ya eneo hili yana uhusiano na kuathiriana. Tishio dhidi ya sehemu moja ya mhimili wa Muqawama linaweza pia kuathiri usalama wa sehemu nyingine.

Akirejelea onyo alilolitoa katika moja ya mikutano maalumu iliyofanyika baada ya operesheni ya tarehe 7 Oktoba, kuhusu madhara ambayo kuanguka kwa Ghaza kungeweza kuwa nayo kwa usalama wa Tehran, alisisitiza kuwa; matukio yaliyofuata yalionesha kuwa vitisho haviishii katika eneo moja pekee. Aliongeza kuwa; ili kukabiliana na vitisho hivyo, ni lazima kuimarisha mtazamo wa pamoja na mkakati wa pamoja ndani ya mhimili wa Muqawama.

Hatua za Kisheria Zinaweza Kukamilisha Nguvu za Kijeshi za Mhimili wa Muqawama

Mhadhiri huyo wa sheria za kimataifa, huku akieleza kuwa kukabiliana na adui hakupaswi kutegemea nyenzo za kijeshi pekee, alisema: Uwezo wa sheria za kimataifa na ufuatiliaji wa mashauri ya kimahakama unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na adui, sawa na nyenzo za kijeshi, na hata katika baadhi ya mazingira unaweza kuwa na ufanisi mkubwa zaidi kuliko nyenzo hizo.

Akizungumzia ushirikiano wake na wanasheria na mawakili wa kimataifa wenye dini na mitazamo mbalimbali, aliongeza kuwa; wanasheria wengi huru duniani wako tayari kuchukua msimamo dhidi ya jinai za Marekani na utawala wa Kizayuni, na kuunga mkono juhudi za kudai haki za mataifa yanayodhulumiwa kupitia njia za kisheria.

Mwisho, Sheikh al-Nasiri alitaka kuandaliwa mpango wa utekelezaji utakaohusisha uwekaji wa kumbukumbu za jinai, uandaaji wa mashauri ya kisheria, uratibu wa familia za mashahidi na ufuatiliaji wa malalamiko katika mahakama za ndani na za kimataifa. Alisisitiza kuwa lengo la mikutano ya aina hii linapaswa kuwa kufikia mbinu na suluhisho za vitendo zitakazowezesha kuwatia hatiani wahalifu na kutetea haki za mataifa yanayodhulumiwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha